.

Saturday, May 14, 2011

SINDANO ZAWAUMBUA ARSERNAL.

PAUL Merson ameibua zengwe katika klabu ya Arsenal, baada ya kudai kwamba walikuwa wakidungwa sindano za dawa zisizojulikana kila wanapokabiliwa na mechi ngumu.
Nyota huyo wa zamani wa England, Merson, alisema hilo lilikuwa likitokea alipokuwa akikichezea kikosi hicho kinachonolewa na Mfaransa Arsene Wenger.
Katika mahojiano maalumu aliyofanya na jarida la soka la Ufaransa la So Foot, Merson alibainisha kwamba walikuwa wakifanyiwa mambo kama hayo walipokuwa Highbury.
Merson, 43, aliyecheza chini ya Wenger katika msimu wa 1996-97, alisema: “Wakati mwingine, katika mkesha wa mechi kubwa, tunakwenda kambini Holiday Inn huko Islington ambako tunadungwa sindano mikononi zenye dawa tusizozitambua.
“Sijawahi kuuliza swali lolote kuhusu hilo. Kwa kipindi kile tulikuwa tukimwamini kocha, unafanya kila kitu anachotaka wewe ufanye.”
Merson alibainisha kwamba hakujali kitu kwa sababu kwa kipindi hicho yeye binafsi alikuwa chapombe na mtumiaji mzuri wa dawa.
Aliongeza: “Kulingana ilivyokuwa utaratibu wa maisha yangu, ile sikuona ni tatizo kwangu na sikuhofia chochote.”
Merson alibainisha pia kila asubuhi wanapowasili kwenye uwanja wa mazoezi walikuwa wakipewa juisi ya machungwa iliyokuwa imechanganywa na ‘Creatine’.
Creatine inadaiwa kuongeza uwezo wa stamina kwa wachezaji na ndio maana ilikuwa ikitumiwa na Wenger kwa ajili ya wachezaji wake.
Merson, 43, alibainisha kila kitu walichokuwa wakifanya katika kambi ya timu hiyo ya Arsenal akibainisha kwamba wakati mwingine walikuwa wakipewa vidonge vikali vya caffeine kila wanapokwenda kucheza mechi za ligi za ugenini.
Katika kikosi hicho cha Arsenal, Merson alicheza zaidi ya mechi 400 na aliweka wazi hakuijua dawa ya njano iliyokuwa ikitumika kuwadunga kabla ya kushuka dimbani kumenyana kwenye mechi kubwa za Ligi Kuu.

No comments:

Post a Comment