.

Saturday, May 14, 2011

"MIMI NA SIMBA SC BASI"

OFISA Habari wa Simba, Clifford Ndimbo, ameachia ngazi kutokana na kile alichodai kutopata ushirikiano na uongozi wa klabu hiyo.
Ndimbo jana aliwasilisha barua ya uamuzi wake huo kwa uongozi wa klabu hiyo yenye maskani yake katika Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam.
Ndimbo bado alikuwa na mkataba na Simba, uliotarajiwa kumalizika Septemba mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ndimbo alisema kuwa uamuzi huo ni wake binafsi na kwamba hajashawishiwa na mtu yeyote yule.
“Nashukuru kuwa nimefanya kazi nzuri wakati wa uongozi uliopita chini ya Mwenyekiti Hassan Dalali iliyopelekea uongozi wa sasa chini ya Mwenyekiti Ismail Rage kuhitaji kuendelea kupata huduma yangu,” alisema.
Ndimbo alisema: “Kwa kipindi chote ambacho nimekaa na uongozi uliopo madarakani, nimekuwa nikitekeleza majukumu yangu, japo wakati mwingine ni katika ugumu ambao nilipohoji, niliambiwa yote yatatatuliwa.”
Ndimbo alishawahi kuandika barua kama hiyo Aprili 5, mwaka huu na kujadiliwa na Kamati ya Utendaji ya Simba, kabla ya kuzuiliwa na Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Evodius Mtawala.
“Pamoja na uamuzi wake huo wa awali kuzuiliwa na Mtawala, hali ya kutoshirikishwa katika matukio ya klabu hiyo, iliendelea kama kawaida, ikiwamo Machi 28, mwaka huu, ambako katika kikao kilichofanyika Makao Makuu yao, hakushirikishwa na uongozi huo.
“Kudharauliwa na kutoshirikishwa…nimeonekana sina maana ndani ya Simba, hivyo uamuzi huu ni kutoka moyoni na somo kubwa kwangu,” alisema.
Wakati Ndimbo akitangaza kuachia ngazi, Ismail Rage alisema hana taarifa na kwamba yeye si mwajiri wake, bali ni Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Evodius Mtawala.
“Ni cheo kidogo sana cha Ndimbo, hivyo hakiniumizi kichwa na nilipowasiliana na Katibu kuhusiana na taarifa hizi, aliniambia hana taarifa,” alisema Rage.

No comments:

Post a Comment