.

Monday, May 16, 2011

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema dawa pekee ya kumaliza tatizo la umaskini uliokithiri miongoni mwa Watanzania wengi nchini ni kuondoa ukiritimba na ufisadi. Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama hicho Taifa, Wilfred Lwakatare, alisema hayo alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Mgazini, Kata ya Kilagano, Wilaya Songea Vijijini, mkoani Ruvuma jana. Mkutano huo ni wa kwanza kati ya mikutano mitatu ya hadhara iliyofanywa na Lwakatare, uliofuatiwa na ule alioufanya katika kituo cha mabasi cha mjini Peramiho na katika Uwanja wa Shule ya Msingi ya Lilambo, Songea mjini.

Lwakatare ni miongoni mwa viongozi waandamizi wa Chadema walioko katika timu sita zinazoendesha operesheni maalum ya chama hicho nchini inayohusisha maandamano.

SIMBA USO KWA USO NA WAARABU?

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika, Simba wamepangwa kundi moja na Ahly ya Misri katika michuano hiyo hatua ya Ligi.

Hata hivyo, Simba itacheza hatua hiyo endapo itaifunga Wydad Casablanca ya Morocco katika mechi itakayochezwa wiki ijayo mjini Khartoum, Sudan.

Shirikisho la Soka Afrika (CAF) imeipa Simba nafasi hiyo na kuiondoa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya kushinda rufaa yake dhidi ya Mazembe kwa kumchezesha Janvier Besala Bokungu Machi mwaka huu huku ikiwa bado haijakamilisha taratibu za usajili wake.

Kwa mujibu wa droo ya michuano hiyo, Simba ikishinda itakuwa kundi B pamoja na Ahly, EST ya Tunisia na Moloudia Club d’Alger ya Algeria wakati kundi A kuna timu za Al Hilal ya Sudan, Coton Sport Garoua ya Cameroon, Raja ya Morocco na mabingwa wa zamani Enyimba ya Nigeria.

Wakati huo huo, uongozi wa Mazembe, umesema utakata rufaa kupinga kuondolewa kwao kwenye michuano hiyo.

Mmiliki wa Mazembe, Moise Katumbi aliiambia BBC jana: “Tumeshtushwa sana Mazembe kuondolewa, tunafahamu uongozi wetu ni safi,” alisema.

Mazembe imeondolewa kwenye michuano ikiwa tayari imeshafuzu hatua ya makundi. Imetwaa ubingwa wa Afrika miaka miwili mfululizo na kufika fainali za Klabu Bingwa ya Dunia ambapo ilifungwa mabao 3-0 na Inter Milan ya Italia.

Wakati hayo yakiendelea, tayari kocha mpya wa Simba Mosses Bassena anatarajia kuanza mazoezi na kikosi chake leo kujiandaa na mechi dhidi ya Casablanca.

Bassena aliyasema hayo Dar es Salaam jana na kwamba walishatuma taarifa kwa wachezaji wao waliokuwa nje ya nchi kwa mapumziko kwamba warudi kwa maandalizi ya mechi hiyo.

Wakati huo huo, Simba jana ilifanya mkutano mkuu wa mwaka na wanachama kuridhia kupitisha bajeti ya shilingi milioni 250 kwa usajili wa wachezaji wa kikosi cha timu hiyo kwa msimu wa ligi ya soka ya Tazania Bara 2011/2012 pamoja na michuano ya Kombe la Shirikisho.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage aliwaambia wanachama kuwa Simba inatarajia kusajili wachezaji wanne wa kimataifa akiwemo mlindamlango wa timu ya Taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’, washambuliaji kutoka Afrika Magharibi katika nchi za Nigeria, Ghana na Cameroon.

"ETI FUSO ZA MBOE NI CHAKAVU?"

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Marando amesema kuwa chama ndicho kilichomwomba Mwenyekiti wake Freeman Mbowe awauzie magari hayo ambayo CCM inayaita chakavu, “Mimi mwenyewe nilihusika kumwomba Mbowe atupe magari yale, akakubali. Baada ya hapo Kamati Kuu iliunda kamati ya watu wanne chini ya makamu mwenyekiti Zanzibar Mohamed Issa kumwomba mwenyekiti akiachie chama magari hayo.
 Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa CHADEMA, Anthony Komu akasema magari hayo hayawezi kufananishwa na magari mengine ya FUSO yanayotembea mitaani kwa kuwa hiyo ni mitambo maalumu yenye vipaza sauti vyenye thamani ya shilingi milioni 222/= na majenereta matatu ambayo kila moja lina thamani ya shilingi milioni 47/=, “Katika magari hayo kuna vipaza sauti (Public addressing system 3 sets) zenye thamani ya dola za Marekani 148,000 (shilingi milioni 222), jenereta tatu kila moja  shilingi milioni 15.5 sawa na shilingi 47,000,000/=”

Komu alisema kila gari lina bodi maalumu yenye uwezo wa kubeba watu wasiopungua 12, jenereta moja kubwa, mafuta ya helkopta, jukwaa la kuhutubia na vifaa vya matangazo ambazo zote zimejengwa kwa shilingi milioni 48.4/=

FREEMASONS YATUA TANZANIA.

UJIO wa Taasisi ya Freemasons nchini na kufanyika kwa mkutano wao jijini Dar es Salaam, umezua mjadala miongoni mwa Watanzani ambapo imedaiwa jamii hiyo imeiteka Dunia.
“Alama kubwa za Freemasons ni nyoka, nyota, minara mirefu, jicho na mwenge, kuna majengo mengi sehemu mbalimbali duniani ambayo yanajengwa na kuwekwa alama hizo bila wenyewe kujua au huku wakijua,” alisema mtabiri mashuhuri nchini Sheigh Yahaya Husein.

Akifafanua zaidi, mnajimu huyo alisema alama hizo zinawekwa kwenye noti, minara, nembo mbalimbali katika nchi tofauti bila wenyewe kujua au wakati mwingine wakiwa wanajua.

“Majengo mengi ya bunge yana minara juu kwa mfano hili la kwetu jipya pale Dodoma, au katika majengo ya mabunge ya Kenya, Ujerumani, Marekani, Canada, Romania, Hungary na Uingereza ambalo lina minara mingi sana, je mmewahi kuuliza kwanini yanajengwa hivyo?” Alihoji mnajimu huyo.

Alisema alama ya Freemasons ya nyoka inatumika katika taasisi nyingi za ndani ya nchi au za kimataifa, akatoa mfano wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hata katika noti ya Tanzania ya shilingi mia tano.

“Kwenye noti alama za Freemasons zipo nyingi kwa mfano Dola za Kimarekani zina alama ya nyota na hata katika noti zetu hapa nyumbani ipo, imewekwa kitaalamu sana katika noti ya shilingi mia tano,” alisema.

Alipoulizwa kama Freemasons inahusika na dini ya mashetani, mnajimu huyo alisema anavyofahamu ni kuwa asili yao ni taasisi nyingine iliyokuwa ikiitwa Skull and Bones (Fuvu na Mifupa) ambayo ilikuwa ikiabudu mashetani na kutoa kafara ya damu
.
“Hili tunalisema kwani hata Babu yake Rais wa zamani wa Marekani, George Bushi aitwae Peasscot S. Bush aliyezaliwa mwaka 1895 na kufa 1972 alikuwa mwanachama, mnaweza kupata haya katika mitandao mbalimbali, siyo siri,” alifafanua na kuongeza kuwa Freemasons ina wanachama matajiri na kwamba ni nadra sana kukuta mlalahoi.

Hata hivyo, katika mahojiano na mwandishi mmoja wa gazeti moja nchini miaka mitatu iliyopita Kiongozi wa Freemasons Afrika Mashariki, Jayantilal Chande alisema taasisi yake haihusiki kabisa na dini ya mashetani kama watu wanavyofikiria na badala yake inajihusisha na kuhudumia jamii kimaendeleo katika nyanja mbalimbali.