.

Wednesday, April 27, 2011

LIL WAYNE: NITASTAAFU NIKIFIKISHA MIAKA 35

Rapper mkali kutoka nchini Marekani,Lil Wayne ambaye amekuwa katika game tangu akiwa na umri wa miaka 15 tayari ameanza kuzungumzia kustaafu mara atakapofikisha umri wa miaka 35. Lil Wayne ambaye miongoni mwa wafuasi wake kupitia label yake ya  Young Money ni pamoja na Rapper mkali mzaliwa wa Toronto,Canada na rapper machachari wa kike,Nicki Minaj, hivi sasa ana umri wa miaka 28. Kwa maana hiyo Rapper huyo ana miaka mingine 7 tu kusimama imara katika ulingo wa muziki.
Akizungumza na Angie Martinez wa Hot 97, Lil Wayne ambaye mashabiki wake hupenda kumwita “Weezy” alieleza kwamba atahakikisha anajituma kwa kadri ya uwezo wake ili kupumzika atakapotimiza miaka 35. “Hiki ndicho kinachotokea unapofanya kazi sana.Watu wanadhani kwamba unaposema unafanya kazi sana ni kwamba unafanya kazi masaa mawili ya ziadaHaya ni maisha yangu, “alisema. “Ndio maana kustaafu katika umri wa miaka 35 ni sawa sawia kabisa kwangu”
Wakati wasanii wenzake kadhaa waliwahi kutangaza kustaafu na kisha kurudi kwenye game ,kama vile Jay-Z, Lil Wayne anaweka bayana kwamba yeye hatanii anaposema hivyo. “Huu ni mpango madhubuti kabisa na nitautekeleza, ”
Alipoulizwa kama ana mpango wa kuendelea kupata watoto wengine, rapper huyo aliweka wazi kwamba hana mpango huo,”Hapana,nipo sawa kwa sasa.Nina watoto wanne na nadhani wananitosha kwa wakati huu”
Hivi sasa Lil Wayne yupo katika tour “I am Music II tour” pamoja na Nicki Minaj, Rick Ross na Travis Barker na anatarajiwa kuachia album yake mpya ya The Carter IV tarehe 16 Mei mwaka huu.

MAWAZIRI TANZANIA: UNAONAJE UTENDAJI WAO...SO FAR?

Msomaji mwenzetu mmoja hapo jana aliomba kuona picha ya Baraza la Mawaziri la sasa baada ya kuona picha ya Baraza la Kwanza la Mawaziri baada ya Muungano katika post iliyopo hapo chini inayomzungumzia Oscar Kambona na Wikipedia.
Kwa bahati mbaya,hatuna picha ya Baraza la Mawaziri lililopo madarakani hivi sasa wakiwa wamesimama au kuketi pamoja. Badala yake tunayo picha hii ambayo tuliitengeneza wenyewe ya Baraza la Mawaziri lililopo madarakani.Kuna fununu kwamba siku si nyingi,Rais Kikwete atafanya mabadiliko katika baraza la mawaziri lililopo.
Sasa badala ya kuweka tu picha na kusema “pichani ni Baraza la Mawaziri na kisha kutoka kushoto kwenda kulia ni yule na yule na yule’,nadhani ni wakati muafaka tukajiuliza,Je unaonaje utendaji wa Mawaziri hawa mpaka hivi sasa?Yupi ambaye unaona anafanya kazi yake ipasavyo na yupi analegalega au kutowajibika kabisa.

OSCAR KAMBONA: MAISHA YAKE KWA MUJIBU WA WIKIPEDIA

Mwaka juzi niliandika kidogo kuhusu umuhimu wa kuandika na kutunza historia zetu hususani mitandaoni katika zama hizi za maendeleo makubwa na ya kasi ya sayansi na tekinolojia.
Nakumbuka niliandika na kuomba wajuzi wa historia ya nchi yetu,kushiriki katika kuandika na kuitunza historia ya Mwanasiasa Mkongwe,Hayati Bibi Titi Mohammed kupitia mradi wa Wikipedia ambao leo hii unasifika na kuaminika kuwa chanzo cha maarifa mbalimbali.Kwa bahati mbaya,mpaka hivi leo ukurasa wa Bibi Titi Mohammed katika Wikipedia bado una mapungufu.Unahitaji kuendelezwa.Ni kweli kwamba hakuna anayejua kwamba Bibi Titi alizaliwa wapi na kwamba hata tarehe yake ya kuzaliwa haijulikani zaidi ya kwamba alizaliwa mwaka 1926?
Pamoja na utata ambao umekuwa ukijitokeza mara kadhaa kuhusu usahihi wa kinachoandikwa katika Wikipedia,hivi leo inasemekana kwamba wanafunzi wengi,hupata maarifa yao kupitia Wikipedia.
Utata unaojitokeza kuhusu usahihi au kinyume chake katika Wikipedia, unatokana na ukweli kwamba Wikipedia inaandikwa na kila mtu.Wewe na mimi.Kila mtu ana uhuru wa kujiunga na Wikipedia na kuchangia.
Hatari ya uhuru huo ni kwamba kuna uwezekano mkubwa wa mtu au watu kuandika historia katika jinsi ambayo itakidhi mahitaji yao na hivyo kuandika habari potofu au za uongo.Hilo linaweza kufanyika kwa bahati mbaya au makusudi.
Kama hunipendi mimi Jeff Msangi,basi unaweza ukaingia katika Wikipedia na kuandika unachokitaka wewe mpaka hapo mwingine anayeijua historia yangu kwa jicho lingine,atakapoingia na kusahihisha.Kama mimi mwenyewe nipo hai pia naweza kuwaandikia Wikipedia na kutoa malalamiko yangu na wao watarekebisha.Kwa kawaida,mtu binafsi haruhusiwi kujiunga na Wikipedia na kuandika habari zake binafsi kwa minajili ya kujitangaza na mambo kama hayo.Historia yako inaandikwa na watu wengine.
Sikumbuki nilikuwa nawaza nini leo nilipoamua kujaribu kutafuta habari zinazomhusu Mwanasiasa mkongwe,Marehemu Oscar Kambona(13th August 1928-July 1997). Historia yake,kwa mujibu wa Wikipedia, imeandikwa vizuri na kwa umakini.Nasema kwa umakini kwa sababu imeandikwa kwa nia ya makusudi ya kuelezea maisha ya mwanasiasa huyo katika miale ya kumtaka msomaji kuelewa vizuri historia yake na kile kilichojiri mpaka akaja  kutoelewana na serikali ya awamu ya kwanza  na bila shaka Hayati Baba wa Taifa,Julius Kambarage Nyerere mwenyewe. Lakini kila kitu kilichoandikwa pale ni sahihi? Mtiririko ule wa matukio ndivyo ulivyokuwa? Ni kweli kwamba Kambona na Nyerere walishindwa kuelewana katika suala zima la siasa za Ujamaa na Azimio la Arusha peke yake? (Nyerere aliamini katika Ujamaa wakati Kambona aliamini katika Ubepari)

KIKWANGUA ANGA KINAKUJA TANZANIA


UJENZI USHAANZA HAPO KWA CHINI



TATU WAJIDANGANYA TABORA JAZZ BAND


Kheri iwe kwako msomaji.Natumaini hujambo na wiki hii haikuwa mbaya kwako.Kama ilikuwa na mikwaruzo,basi ni ile ambayo unaweza kuikabili.Kama ilikuwa ngumu sana,basi mwachie Muumba.Yeye anaweza.
Hii ni weekend ya katikati mwa mwezi. Hapa tunaweza kusema kama hesabu za mwanzo wa mwezi zilikwenda kombo,basi leo tanki la mafuta lipo chini ya mstari wa katikati.Usitie shaka,wenzako wakikupigia simu kwamba muongozane kwenda viwanjani,tia  kisingizio cha “dozi ya malaria”. Si unajua hakuna kitu kibaya kama kwenda mahali na kuanza kutumbua huku hesabu kali zikiendelea kichwani.Unaweza kabwa na mnofu wa nyama.Kile kicheko cha bar ya kona kinaota mbawa. Zile mbwembwe za “tuletee kama tulivyo na kisha mwambie jamaa wa jikoni aje” leo sio mahala pake.
Ushauri wangu;weekend hii tumia muda wako nyumbani.Cheza na wanao.Soma nao,cheka nao. Hilo likikushinda (yawezekana hujazoea au watoto wana ratiba zingine za birthday parties nk, basi jisomee.Kama unacho kitabu cha After  4:30 cha David G.Mailu kikamate uso. Kuwa makini,kilipigwa marufuku. Sishauri kukamata remote na kuanza kubadili channel. Ina raha gani kushinda kutwa  ukitazama wenzako wanafanya wanachokipenda na kulipwa ilhali wewe chali?! Aste aste,msaada kwenye tuta.Vyovyote vile iwavyo, usikate tamaa,ni life.Kuna leo na kuna kesho. Unaweza lala masikini ukaamka tajiri.Cheza karata zako vyema.Jitokeze mahali sahihi katika wakati sahihi au muafaka.
Leo katika Zilipendwa tunaelekea Tabora.Kule tunawakuta Tabora Jazz Band.Miaka mingi imeshapita tangu nitembelee mkoa wa Tabora. Leo hii sina hata kumbukumbu nzuri kwamba mara ya mwisho kufika pale ilikuwa lini.Pamoja na hayo, bado ninakumbuka kwamba niliupenda ule mji.Enzi zile,ulikuwa ni mji simple usio na mengi.Watu walijuana vyema.Nakumbuka Chuo cha Uhazili.Kilisifika kwa kutoa makatibu muhtasi wa “ukweli”.Mama zangu wadogo kadhaa wamesoma pale.Nakumbuka shule ya sekondari Uyui.Nilikwenda pale kumsalimia mjomba wangu alipokuwa anasoma pale. Nakumbuka Tabora Girls na Tabora Boys. Mpaka hivi leo nina ndugu wanaishi maeneo ya kule. Nakumbuka disco la pale.Mwana Isungu.Hospitali ya Kitete.Tabora,Tabora,Tabora…nitarudi.
Tukiachana na kumbukumbu yangu inayofifia kuhusu Tabora,Tabora Jazz Band wanao wimbo unaoitwa Tatu Wajidanganya. Kwamba Tatu anadhani kwa sababu anapendwa,basi anayo nguvu ya kumgombanisha jamaa na ndugu zake.Penzi likashinda undugu.Inawezekana?
Wimbo huu ni miongoni mwa zile nyimbo ambazo kwa namna fulani zilikuwa zinatupa kitambulisho cha muziki wa kitanzania ambao ulikuwa ni mchanganyiko mzuri sana wa Afro-Jazz au Afro-Cuban.Jaribu kusikiliza jinsi ala zilivyopangwa.Piga picha jinsi jamaa walivyokuwa jukwaani na zile bugaloo zao.Burudani ya kutosha.Basi burudika  na Tatu Wajidanganya na uwe na weekend njema

JAMANI MTUSAIDIE KUJENGA DARAJA HUKU KWETU

Wakazi wa Dar es Salaam wakivuka Mto Tegeta wakiwa wamebebana baada ya daraja linalounganisha Salasala Kilimahewa na kulangwa Goba kubomoka.