.

Saturday, May 14, 2011

"NIACHENI NA YANGA YANGU JAMANI"

HATIMAYE mshambuliaji wa FK Jagodina ya Serbia, Mghana Kenneth Asamoah, ametua rasmi jijini Dar es Salaam  na kulakiwa na viongozi, wanachama na wapenzi wa Yanga kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Baada ya kutua kwenye uwanja huo, viongozi wa Yanga walikwenda naye moja kwa moja katika Makao Makuu yao yaliyopo katika makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga, jijini, kwa ajili ya kufanya naye mazungumzo ya mwisho ya kuichezea timu hiyo msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa.
Mchezaji huyo aliyeteka vichwa vya vyombo vya habari kwa siku za hivi karibuni hapa nchini, aliwasili saa 3:30 asubuhi.
Yanga ilijaribu kumsajili Assamoah kwa ajili ya msimu uliopita, lakini ilishindwa kumtumia kutokana na kukwama kwa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) na hivyo kurejea katika klabu yake ya FC Jagodina, iliyomtoa kwa mkopo.
Na kutokana na kiwango alichokionyesha wakati wa mechi za maandalizi ya msimu uliopita, Yanga wameamua kumfuatilia tena ambapo Mghana huyo ameonyesha nia ya kukipiga Jangwani msimu ujao.
Lakini wakati Yanga wakiendelea na mchakato wao wa kumnasa Assamoah, hivi karibuni, watani wao wa jadi, Simba, walitangaza nia yao ya kuwania saini ya mshambuliaji huyo.
Wekundu wa Msimbazi hao, walifika mbali katika mchakato wao huo, wakidai kuwa jitihada zinazofanywa na Yanga, zitageuka kilio baada ya kufungwa kwa dirisha la usajili wa msimu ujao kwa kuwa watani wao hao wanatumia njia ya mkato.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage, aliwaambia waandishi wa habari katikati ya wiki hii kuwa wao wanamfuatilia Assamoah kwa kufuata sheria za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kuzungumza na klabu ya mchezaji kwanza badala ya kuanza na mchezaji kama wanavyofanya Yanga.
Rage alisema kuwa kinachofanywa na Yanga kinaweza kuigharimu klabu hiyo iwapo Jagodina watashitaki FIFA na mwisho wa siku, watani wao wa jadi hao, wataishia kunawa.
Kauli hiyo ya Rage ilionekana kuwachanganya wapenzi wa Yanga, wakihisi huenda klabu yao ‘ikaingia mkenge’ kwa Assamoah kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Hatimaye jana Assamoah alikata mzizi wa fitina baada ya kutua Jangwani na kusema: “Nimekuja kulipa fadhila Yanga kwa kuwa msimu uliopita klabu hii ilionyesha upendo mkubwa kwangu.”
Alisema Yanga ni timu ambayo anaamini ina umoja na mshikamano, hivyo hiyo ni bahati kwake kuchezea timu hiyo na hayupo tayari kujiunga na timu yoyote nchini hata kwa uhamisho wa fedha nyingi.
Aliwaahidi mashabiki wa timu hiyo kuwa msimu ujao atahakikisha anarudisha ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza Agosti, mwaka huu.
“Ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba nitajitahidi sana uwanjani kama ishara ya kuipenda timu yangu ya Yanga,” alisema Assamoah huku akionekana kuwa na furaha isiyo kifani.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga, alisema kuwa ni vigumu timu yoyote kumchukua mchezaji huyo, kwa kile alichodai kuwa bado wana makubaliano na timu anayochezea (Jagodina) kwa sasa.
“Kwa uwezo alionao Kenneth Assamoah, tuna mpango wa kumpa mkataba wa zaidi ya miaka mitatu,” alisema Nchunga.
Kenneth Asamoah, alizaliwa mwaka 1988 katika Mji wa Kumasi, nchini Ghana, ambapo mwaka 2006 alijiunga na Asante Kotoko ya huko na kuichezea kwa miaka miwili kabla ya kujiunga na FK Jagodina inayoshiriki Ligi Kuu ya Serbia ‘Super Liga’.

No comments:

Post a Comment