.

Monday, May 16, 2011

SIMBA USO KWA USO NA WAARABU?

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika, Simba wamepangwa kundi moja na Ahly ya Misri katika michuano hiyo hatua ya Ligi.

Hata hivyo, Simba itacheza hatua hiyo endapo itaifunga Wydad Casablanca ya Morocco katika mechi itakayochezwa wiki ijayo mjini Khartoum, Sudan.

Shirikisho la Soka Afrika (CAF) imeipa Simba nafasi hiyo na kuiondoa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya kushinda rufaa yake dhidi ya Mazembe kwa kumchezesha Janvier Besala Bokungu Machi mwaka huu huku ikiwa bado haijakamilisha taratibu za usajili wake.

Kwa mujibu wa droo ya michuano hiyo, Simba ikishinda itakuwa kundi B pamoja na Ahly, EST ya Tunisia na Moloudia Club d’Alger ya Algeria wakati kundi A kuna timu za Al Hilal ya Sudan, Coton Sport Garoua ya Cameroon, Raja ya Morocco na mabingwa wa zamani Enyimba ya Nigeria.

Wakati huo huo, uongozi wa Mazembe, umesema utakata rufaa kupinga kuondolewa kwao kwenye michuano hiyo.

Mmiliki wa Mazembe, Moise Katumbi aliiambia BBC jana: “Tumeshtushwa sana Mazembe kuondolewa, tunafahamu uongozi wetu ni safi,” alisema.

Mazembe imeondolewa kwenye michuano ikiwa tayari imeshafuzu hatua ya makundi. Imetwaa ubingwa wa Afrika miaka miwili mfululizo na kufika fainali za Klabu Bingwa ya Dunia ambapo ilifungwa mabao 3-0 na Inter Milan ya Italia.

Wakati hayo yakiendelea, tayari kocha mpya wa Simba Mosses Bassena anatarajia kuanza mazoezi na kikosi chake leo kujiandaa na mechi dhidi ya Casablanca.

Bassena aliyasema hayo Dar es Salaam jana na kwamba walishatuma taarifa kwa wachezaji wao waliokuwa nje ya nchi kwa mapumziko kwamba warudi kwa maandalizi ya mechi hiyo.

Wakati huo huo, Simba jana ilifanya mkutano mkuu wa mwaka na wanachama kuridhia kupitisha bajeti ya shilingi milioni 250 kwa usajili wa wachezaji wa kikosi cha timu hiyo kwa msimu wa ligi ya soka ya Tazania Bara 2011/2012 pamoja na michuano ya Kombe la Shirikisho.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage aliwaambia wanachama kuwa Simba inatarajia kusajili wachezaji wanne wa kimataifa akiwemo mlindamlango wa timu ya Taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’, washambuliaji kutoka Afrika Magharibi katika nchi za Nigeria, Ghana na Cameroon.

No comments:

Post a Comment