Kheri iwe kwako msomaji.Natumaini hujambo na wiki hii haikuwa mbaya kwako.Kama ilikuwa na mikwaruzo,basi ni ile ambayo unaweza kuikabili.Kama ilikuwa ngumu sana,basi mwachie Muumba.Yeye anaweza.
Hii ni weekend ya katikati mwa mwezi. Hapa tunaweza kusema kama hesabu za mwanzo wa mwezi zilikwenda kombo,basi leo tanki la mafuta lipo chini ya mstari wa katikati.Usitie shaka,wenzako wakikupigia simu kwamba muongozane kwenda viwanjani,tia kisingizio cha “dozi ya malaria”. Si unajua hakuna kitu kibaya kama kwenda mahali na kuanza kutumbua huku hesabu kali zikiendelea kichwani.Unaweza kabwa na mnofu wa nyama.Kile kicheko cha bar ya kona kinaota mbawa. Zile mbwembwe za “tuletee kama tulivyo na kisha mwambie jamaa wa jikoni aje” leo sio mahala pake.
Ushauri wangu;weekend hii tumia muda wako nyumbani.Cheza na wanao.Soma nao,cheka nao. Hilo likikushinda (yawezekana hujazoea au watoto wana ratiba zingine za birthday parties nk, basi jisomee.Kama unacho kitabu cha After 4:30 cha David G.Mailu kikamate uso. Kuwa makini,kilipigwa marufuku. Sishauri kukamata remote na kuanza kubadili channel. Ina raha gani kushinda kutwa ukitazama wenzako wanafanya wanachokipenda na kulipwa ilhali wewe chali?! Aste aste,msaada kwenye tuta.Vyovyote vile iwavyo, usikate tamaa,ni life.Kuna leo na kuna kesho. Unaweza lala masikini ukaamka tajiri.Cheza karata zako vyema.Jitokeze mahali sahihi katika wakati sahihi au muafaka.
Leo katika Zilipendwa tunaelekea Tabora.Kule tunawakuta Tabora Jazz Band.Miaka mingi imeshapita tangu nitembelee mkoa wa Tabora. Leo hii sina hata kumbukumbu nzuri kwamba mara ya mwisho kufika pale ilikuwa lini.Pamoja na hayo, bado ninakumbuka kwamba niliupenda ule mji.Enzi zile,ulikuwa ni mji simple usio na mengi.Watu walijuana vyema.Nakumbuka Chuo cha Uhazili.Kilisifika kwa kutoa makatibu muhtasi wa “ukweli”.Mama zangu wadogo kadhaa wamesoma pale.Nakumbuka shule ya sekondari Uyui.Nilikwenda pale kumsalimia mjomba wangu alipokuwa anasoma pale. Nakumbuka Tabora Girls na Tabora Boys. Mpaka hivi leo nina ndugu wanaishi maeneo ya kule. Nakumbuka disco la pale.Mwana Isungu.Hospitali ya Kitete.Tabora,Tabora,Tabora…nitarudi.
Tukiachana na kumbukumbu yangu inayofifia kuhusu Tabora,Tabora Jazz Band wanao wimbo unaoitwa Tatu Wajidanganya. Kwamba Tatu anadhani kwa sababu anapendwa,basi anayo nguvu ya kumgombanisha jamaa na ndugu zake.Penzi likashinda undugu.Inawezekana?
Wimbo huu ni miongoni mwa zile nyimbo ambazo kwa namna fulani zilikuwa zinatupa kitambulisho cha muziki wa kitanzania ambao ulikuwa ni mchanganyiko mzuri sana wa Afro-Jazz au Afro-Cuban.Jaribu kusikiliza jinsi ala zilivyopangwa.Piga picha jinsi jamaa walivyokuwa jukwaani na zile bugaloo zao.Burudani ya kutosha.Basi burudika na Tatu Wajidanganya na uwe na weekend njema
No comments:
Post a Comment