.

Wednesday, April 27, 2011

OSCAR KAMBONA: MAISHA YAKE KWA MUJIBU WA WIKIPEDIA

Mwaka juzi niliandika kidogo kuhusu umuhimu wa kuandika na kutunza historia zetu hususani mitandaoni katika zama hizi za maendeleo makubwa na ya kasi ya sayansi na tekinolojia.
Nakumbuka niliandika na kuomba wajuzi wa historia ya nchi yetu,kushiriki katika kuandika na kuitunza historia ya Mwanasiasa Mkongwe,Hayati Bibi Titi Mohammed kupitia mradi wa Wikipedia ambao leo hii unasifika na kuaminika kuwa chanzo cha maarifa mbalimbali.Kwa bahati mbaya,mpaka hivi leo ukurasa wa Bibi Titi Mohammed katika Wikipedia bado una mapungufu.Unahitaji kuendelezwa.Ni kweli kwamba hakuna anayejua kwamba Bibi Titi alizaliwa wapi na kwamba hata tarehe yake ya kuzaliwa haijulikani zaidi ya kwamba alizaliwa mwaka 1926?
Pamoja na utata ambao umekuwa ukijitokeza mara kadhaa kuhusu usahihi wa kinachoandikwa katika Wikipedia,hivi leo inasemekana kwamba wanafunzi wengi,hupata maarifa yao kupitia Wikipedia.
Utata unaojitokeza kuhusu usahihi au kinyume chake katika Wikipedia, unatokana na ukweli kwamba Wikipedia inaandikwa na kila mtu.Wewe na mimi.Kila mtu ana uhuru wa kujiunga na Wikipedia na kuchangia.
Hatari ya uhuru huo ni kwamba kuna uwezekano mkubwa wa mtu au watu kuandika historia katika jinsi ambayo itakidhi mahitaji yao na hivyo kuandika habari potofu au za uongo.Hilo linaweza kufanyika kwa bahati mbaya au makusudi.
Kama hunipendi mimi Jeff Msangi,basi unaweza ukaingia katika Wikipedia na kuandika unachokitaka wewe mpaka hapo mwingine anayeijua historia yangu kwa jicho lingine,atakapoingia na kusahihisha.Kama mimi mwenyewe nipo hai pia naweza kuwaandikia Wikipedia na kutoa malalamiko yangu na wao watarekebisha.Kwa kawaida,mtu binafsi haruhusiwi kujiunga na Wikipedia na kuandika habari zake binafsi kwa minajili ya kujitangaza na mambo kama hayo.Historia yako inaandikwa na watu wengine.
Sikumbuki nilikuwa nawaza nini leo nilipoamua kujaribu kutafuta habari zinazomhusu Mwanasiasa mkongwe,Marehemu Oscar Kambona(13th August 1928-July 1997). Historia yake,kwa mujibu wa Wikipedia, imeandikwa vizuri na kwa umakini.Nasema kwa umakini kwa sababu imeandikwa kwa nia ya makusudi ya kuelezea maisha ya mwanasiasa huyo katika miale ya kumtaka msomaji kuelewa vizuri historia yake na kile kilichojiri mpaka akaja  kutoelewana na serikali ya awamu ya kwanza  na bila shaka Hayati Baba wa Taifa,Julius Kambarage Nyerere mwenyewe. Lakini kila kitu kilichoandikwa pale ni sahihi? Mtiririko ule wa matukio ndivyo ulivyokuwa? Ni kweli kwamba Kambona na Nyerere walishindwa kuelewana katika suala zima la siasa za Ujamaa na Azimio la Arusha peke yake? (Nyerere aliamini katika Ujamaa wakati Kambona aliamini katika Ubepari)

No comments:

Post a Comment