.

Monday, May 2, 2011

KUMBE KUSMA NI KUDHOHOFISHA AKILI!

WASOMI zaidi ya 1,200 katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wamesimamishwa masomo baada ya juhudi za kushinikiza madai yao kugonga mwamba.
Wasomi hao wanalilia vitendea kazi, zikiwamo laptop (kompyuta) ili ziwawezeshe kuendana na dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia.
Niliposikia madai yao sikushangaa. Sikushangaa kwa sababu tumekubali kuwa na jamii inayotaka ilimiwe mashamba, ipandiwe, ivuniwe, iandaliwe chakula, ilishwe; na ikiwezekana isaidiwe kujisaidia, na hata ikibidi kuzoa uchafu, basi wawepo wazoaji!
Sikushangaa kusikia madai ya kutaka “vitendea kazi”, lakini nilipigwa na bumbuwazi kusikia aina ya madai! Madai yao yamenifanya niingie kwenye maduka kuangalia bei za laptop.
Nikaangalia bei ya laptop mpya na zilizokwishatumiwa Ulaya na Marekani. Nikakuta bei ya laptop mpya inaanzisha Sh 700,000. Mitumba inauzwa Sh 400,000 hadi Sh 500,000.
Wasomi wetu wamekuwa na hiari ya kurejea makwao kwa sababu Bodi ya Mikopo imeshindwa kuwapa mikopo kwa ajili ya kununua vifaa hivyo.
Aidha, madai yao yalikolezwa chachandu ya kauli wanayosema ilitolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ya kupewa kompyuta hizo.
Februari, mwaka huu niliandika makala ya kuwaunga mkono Wachina walioingia kwa wingi, si Tanzania tu, bali katika kila nchi katika dunia yetu.
Tunaweza kudhani kuwa wingi wa Wachina hapa nchini unatokana na wingi wao, lakini ukweli ni kwamba ndani ya mioyo na akili za Wachina, kuna kitu cha ziada kinachowafanya wawe wa kugaagaa na upwa!
Wachina wameujua ujasiriamali. Wametii miiko na taratibu zake. Wanajua hawana nafasi ya kwenda kula na kuishi kwa mjomba wala kwa jirani.
Maisha ya Mchina yanatokana na juhudi zake binafsi na nyongeza ya mazingira mazuri ya kuwezeshwa yaliyowekwa na Serikali yao.
Nimepata kuzungumza na Wachina kadhaa wanaofanya kazi ya kusukuma mikokoteni pale Kariakoo jijini Dar es Salaam. Nimezungumza na Wachina wanaofanya kazi nyingi za uchuuzi katika maeneo mbalimbali nchini.
Kati ya wote hao, nilibaini kuwa mwenye elimu ya chini ana elimu ya juu ya sekondari. Huyo ndiye hakusoma. Wengi wana shahada za uzamili na uzamivu.
Fikiria, mtu mwenye shahada ya uzamivu anajishusha hata kukubali kusukuma mkokoteni ili aweze kutengeneza maisha yake. Tena, basi, Wachina wangependa kuona muda wa kufanya kazi, muda wa kufungua na kufunga maduka unakuwa saa 24. Hawataki kupumzika.
Turejee kwa wasomi wetu wa Dodoma. Kudai laptop leo ni aibu kwa msomi wa chuo kikuu. Kudai laptop inayouzwa Sh 500,000 kwa mtu aliyefikia ngazi hiyo ya elimu, ni upuuzi usiokubalika.
Wasomi wa Tanzania ndiyo pekee ambao wakiwa katika vyuo vikuu, hawataki kujishughulisha na kazi za kuwaingizia kipato.
Wasomi wetu wakiingia katika vyuo vikuu wanabadilika na kujiona kuwa na haki ya kutendewa zaidi kuliko kutenda. Usomi ni ubwana na ubibi. Ni u-mangimeza.
Wasomi wa vyuo vya elimu ya juu wanapaswa wabadilike. Waingie madarasani kama kawaida, lakini wawe na muda wa kufanya kazi za ziada za kuwaingia mapato.
Haya ninayoyasema hapa yanafahamika vema mno na Watanzania waliokwenda kusoma ng’ambo. Wengi wanaokwenda huko wanajilipia ada.
Wanajilipia ada kwa ujira wanaopata kutokana na kazi za kuosha sufuria, kusafisha vyoo, kusafisha mabanda ya wanyama, kuchuma matunda, kutunza wazee, kujfagia barabara na kadhalika.
Kwa bahati nzuri kazi mbaya mbaya Ulaya na Marekani malipo yake ni manono. Pengine wasomi Watanzania kwa kutambua kuwa wapo mbali na nyumbani kwao, na hakuna anayewatambua kwa sura, hukubali kuzifanya kazi hizo na kujipatia fedha nyingi.
Tunapoona nyumba au magari ya wasomi wetu walio ughaibuni, tutambue kuwa fedha zilizonunua vitu hivyo zimepatikana kwa shughuli kadha wa kadha, zikiwamo za kuwaosha vikongwe!
Suala la kujitafutia fedha kwa ajili ya maendeleo si la kuonea aibu. Wasomi wetu wa Dodoma na kwingineko nchini hawapo tayari kutumia muda usio wa masomo kufanya kazi ya mapokezi katika hoteli, kufuga kuku, kuuza baa au hotelini, kufagia barabara wala kufanya shughuli yoyote halali ya kuwaingizia fedha.
Matokeo ya malezi haya hatari ndiyo haya tunayoona sasa. Wanafunzi wanadai hata laptop ambazo kimsingi wangeweza kujibidisha wenyewe na kupata fedha za kuwawezesha kuzinunua.
Elimu bado haijawasaidia wasomi wa Tanzania. Kwa Tanzania heri ambaye hakusoma kuliko mtu aliyepata elimu ya chuo kikuu. Wakati wa mgawo mkali wa umeme mwezi Januari na Fabruari mwaka huu nilijifunza kitu kingine kwa wasomi wetu.
Barabara yangu ya kwenda na kutoka kazini ni ile ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Chuo kile kina mandhari nzuri, pengine kuliko chuo chochote katika Afrika. Wakati wa mgawo wa umeme usiku, chuo kile kinatisha! Kinatisha kwa giza nene kutokana na misitu mingi na mizuri iliyokizunguka.
Ajabu ni kwamba nilipokuwa nikipita katika chuo hicho, sikuona dalili yoyote ya mwanga, si kwenye ofisi za maprofesa na madktari, wala katika mabweni yaliyosheheni maelfu ya wanafunzi.
Katika hali ya kawaida ya usomi, chuo kikuu ndio ingekuwa sehemu ya mwisho ya watu kulalamika kukosa umeme. Maelfu ya wanafunzi wanaolala kwenye mabweni yake ni hazina kubwa ya kupata umeme.
Kinyesi kinachotoka kwenye mabweni yale ni chanzo muhimu sana cha nishati. Katika hali ya kawaida ya usomi uliotukuka, sisi wapita njia tungepata faraja kuona umeme ukiwaka kwenye vyumba vya wasomi hao.
Umeme huo ungetokana na nguvu za kinyesi kinachozalishwa na wanafunzi hao. Umeme ambao ungezalishwa hapo bila shaka ungekuwa na uwezo wa kuwasha taa katika vyumba na ofisi zote bila kuwasha viyoyozi.
Sikuwasikia wasomi wetu wa sayansi wakiomba japo fedha za kuwawezesha kuzalisha umeme kwa kutumia teknolojia hiyo ambayo ni nyepesi mno.
Sikuwasikia wala wakijadili namna ya kupata fedha za kuwawezesha kufunga vifaa vya kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za jua.
Maisha ya msomi yanapokuwa ya kijima, sawa na ndugu zetu waishio vijijini, hakuna maana ya kuwa na wasomi. Maisha ya msomi yanapaswa yaonyeshe tofauti kati yake na mtu ambaye hakupata elimu. Kama mwananchi kijiji mwenye ng’ombe wawili anaweza kupata umeme kwa kinyesi cha ng’ombe, iweje hawa wasomi maelfu kwa maelfu kinyesi chao kisitumike kuwasha japo balbu moja?
Kwa wasomi wa Dodoma, kama kweli Waziri Mkuu aliwaahidi kuwa watapata mikopo ya laptop, alipotoka. Miaka minne katika chuo ni mingi. Watafute mashamba ya zabibu walime. Wauze baa wapate fedha.
Kila Jumamosi mjini Dodoma kuna mnada. Wauze nyama na vinywaji vingine ili wajipatie fedha zitakazowawezesha kujinunulia vitu kama laptop.
Serikali ibaki na dhima ya kuhangaikia mambo makubwa makubwa ya majengo, wahadhiri, vifaa vya kujifunzia, fedha za mafunzo kwa vitendo na kadhalika.
Wasomi waingie mitaani wachape kazi kwa bidii kubwa. Wasomi waache kudeka. Wao si watoto wadogo. Wafanye kazi za ziada.
Wapo waliothubutu kufanya hivyo, na mambo yamewaendea vizuri. Bila kubadili tabia hizi za kipuuzi, wasomi wetu watakuwa hawana tofauti na walemavu wanaostahili kutunzwa na jamii.

No comments:

Post a Comment