.

Wednesday, May 18, 2011

FANYA KINWA CHAKO KIWE SAFI NA KUJIKINGA NA MARADHI.



 
Zirostomia (Xerostomia) ni neno la kigiriki litumikalo kwenye tiba kumaanisha hali ya kinywa kikavu (xeros – kavu, stomia – hali ya kinywa) . Udhaifu wa tezi za mate ni tafsiri nyingine ya Zirostomia. Hali ya kinywa kikavu hujitokeza pale mtu anapohisi ukavu wa kinywa kutokana na kupungua kwa mate kinywani. Hakika hali ya kinywa kikavu sio ugonjwa bali ni dalili za ugongwa fulani. Kuwapo kwa dalili hii kunaashiria upungufu wa uzalishwaji wa mate kinywani kwa kiwango fulani

Zirostomia inasababishwa na nini?

Kuna sababu kadhaa zinazosababisha hali ya kinywa kikavu zikiwamo:-
  • Uvutaji wa sigara: hiki ni chanzo kikuu cha hali ya kinywa kikavu
  • Baadhi ya madawa yanayotumika kutibu baadhi ya magonjwa hudhoofisha ufanisi wa tezi mate. Tafiti zinaonesha kuwa zaidi ya aina 400 ya madawa yanayotumika hospitalini husababisha dalili za hali ya kinywa kikavu. Mfano madawa yatumikayo kudhibiti shinikizo la damu, dawa zitumikazo kutibu ugonjwa wa Parkinson, dawa zitumikazo kutibu mzio, dawa za kutibu mafua , dawa zitumikazo kutibu vidonda vya tumbo na baadhi ya dawa za maumivu husababisha hali ya kinywa kikavu.
  • Hali zinazosababisha upungufu wa maji mwilini kama homa, kuvuja jasho kwa wingi, kutapika ama kuharisha kunaweza kusababisha hali ya kinywa kikavu kwa muda.
  • Baadhi ya magonjwa na hali zinazoathiri mwili mzima ikiwamo tezi za mate husababisha hali ya kinywa kikavu i.e. (ugonjwa wa kisukari, ugonjwa wa parkinson, HIV/AIDS etc)
  • Tiba ya kansa (mionzi ama madawa) vinaweza kuharibu tezi za mate na kuathiri uzalishaji na usambazaji wa mate kinywani.
Zirostomia ina athari zipi kwa utunzaji wa afya ya kinywa na meno?

Zirostomia siyo hali ya kawaida. Imezoeleka kuona damu, mkojo na machozi vikitumika kwenye uchunguzi wa hali ya afya na magonjwa. Wakati huo huo mate (sio makohozi) hayapewi uzito kwenye uchunguzi wa afya na magonjwa. Kazi kubwa ya mate ni kulinda na kutunza afya ya kinywa na meno, vile vile yanasaidia kwenye uyeyushaji wa chakula kinywani, kutambua ladha na hata kuongea na kuimba, isitoshe mate ni kiashiria muhimu cha kutambua hatari ya magonjwa yanayoshambulia mfumo wa damu mwilini na hata hali zingine za mwili kama ujauzito.
Hali ya kinywa kikavu hakika sio kitu cha kawaida, na jamii nzima inapaswa kuelimishwa na kutambua hali hii inapotokea na watu wote wanaokuwa na hali ya kinywa kikavu hawana budi kumwona daktari wa meno kwa ushauri na tiba. Wagonjwa wenye hali ya kinywa kikavu ambao hawapati ushauri na tiba ya kudhibiti hali hii mapema mara nyingi wanapata tatizo kubwa la kuoza meno mengi kwa mpigo na kuvimba kwa kuta zizungukazo kinywa na fizi. Matatizo haya hutokea kwa sababu ya upungufu wa mate kinywani ambayo kwa kawaida huwa na vimeng’enya na viasili ambavyo husaidia kinywa kujisafisha chenyewe na hivyo kuzuia kuoza meno na kuvimba kwa fizi na kuta nyinginezo kinywani.

Nitajuaje kuwa naathirika na Zirostomia?

 
Kwa kawaida, tezi za mate ni kama kiwanda hivi. Tezi zinahitaji malighafi , machine na umeme ili kuzalisha mazao yaliyokusudiwa. Ikiwa kutatokea mabadiliko kwenye mchakato na mzunguko wa uzalishaji , ni wazi mazao yaliyokusudiwa hayatatokea.
Tukirudi kwenye tezi za mate, tunafahamu kuwa tatizo lolote litakaloathiri upatikanaji wa metabolites kama maji, kuharibiwa kwa tezi kutokana na ugonjwa ama jeraha, na kudhoofu kwa mfumo wa neva za tezi hupunguza uzalishaji wa mate kinywani.
Hatua za awali za zirostomia zaweza kuwa na dalili kidogo zisizoshtua mgonjwa, hata hivyo kadiri muda unavyoendelea hali inaweza kuwa mbaya zaidi hususani mgonjwa anaposhindwa kula na kuongea vizuri. Hatua hii huenda sambamba na kuhisiwa kwa harufu mbaya kutoka kinywani. Ili kubaini kama Zirostomia imefikia hatua mbaya, uchunguzi wa ufanisi wa tezi za mate hufanyika kwa kukusanya mate (kwa kutumia kifaa maalumu) na kupima kiasi cha mate ambacho mgonjwa anazalisha ndani ya dakika tano. Vipimo vingine vitumikavyo kupima ufanisi wa tezi hufanyika kitaalamu zaidi kwa kutumia Ultrasound mashine tezi ama kwa mionzi maalumu ya tezi za mate (Parotid Sialography).
Tafiti zimeonesha kuwa mmoja kati ya watu wazima wanne hulalamika kuwa na hali ya kinywa kikavu ama kuvimba kwa kuta za kinywa na fizi, matokeo ya utafiti huu yanafanana na ukweli kuwa 40% ya watu wazima hulalamika kuwa na hali ya kinywa kikavu kwa vipindi fulani hivyo kuonyesha kuwa Zirostomia ni tatizo bubu miongoni mwa jamii.

Tiba ya Zirostomia ni nini?

 
Matibabu ya zirostomia inayomkabili mgonjwa yanategemea chanzo chake, baadhi ya njia zitumikazo kutibu Zirostomia ni:-
  • Kunywa maji mengi kudhibiti upungufu wa maji mwilini.
  • Epuka vyakula vyenye caffeine kwa wingi kama kahawa, chai na baadhi ya vyakula vyenye magadi kwa wingi.
  • Epuka uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe kupindukia
  • Tafuna jojo zisizo na sukari ili kuchagiza uzalishwaji mate kinywani
  • Tumia “chinese green tea”, chamomile na ginger kuchagiza uzalishwaji mate.
  • Ikiwa hali ya kinywa kikavu inasababishwa na dawa, tafadhali mwone daktari wa meno kwa ushauri.

No comments:

Post a Comment