Maafisa wa Marekani wamesema kuwa maiti ya Osama bin Laden ilipewa heshima zote na kusaliwa kiislamu kabla ya kuzikwa baharini, lakini maswali mengi yamezuka kwanini azikwe baharini wakati Marekani ingeweza kumzika kwenye ardhi ya sehemu yeyote ile?.
Taratibu za kiislamu zinataka maiti izikwe mapema iwezekanavyo badala ya kucheleweshwa isipokuwa iwapo uchunguzi wa kifo cha mtu aliyefariki utahitajika. Maafisa wa Marekani wanasema kuwa walizingatia sana taratibu za kiislamu kwa kuuzika mwili wa Osama bin Laden ndani ya masaa machache. "Taratibu za mazishi katika dini ya kiislamu zilifuatwa, maiti yake ilifanyiwa taratibu zote za kidini kwenye kambi ya jeshi, mwili wake ulivalishwa sanda nyeupe, uliwekwa ndani ya mfuko uliowekwa vitu vizito ili uweze kuzama baharini na kisha ulidondoshwa kwenye peninsula ya Uarabuni katika bahari ya Hindi. Maafisa wa Marekani walisema kuwa tukio hilo lilitokea masaa 12 baada ya Obama kuuliwa kwa kupigwa risasi ya kichwa. Taarifa ya televisheni ya ABC ilisema Osama alipigwa risasi ya pili kwenye kichwa ili kuhakikisha kuwa amefariki dunia. Mwili wake ulisafirishwa hadi kwenye kambi ya jeshi la Marekani nchini Afghanistan ambapo sampo yake ya DNA ilipimwa ambapo ilionekana kushahibiana kwa asilimia 99 na sampo za ndugu kadhaa wa Osama. Ulichukuliwa na kuwekwa kwenye meli ya kivita ya Marekani, USS Carl Vinson iliyopo kaskazini mwa bahari ya Uarabuni ambapo taratibu za kidini zilifanyika na baadae mwili wake ulizikwa baharini. Marekani ilisema kuwa iliamua kumzika Osama baharini baada ya kukosekana kwa mtu ambaye angeikubali kuizika maiti yake. Iliripotiwa kuwa Saudi Arabia iliukataa mwili wa Osama bin Laden. Hata hivyo kumekuwa na maswali mengi kwanini Marekani iliamua kumzika Osama bin Laden baharini. Kwa mujibu wa imamu Dr Abduljalil Sajid wa Uingereza ambaye pia ni mwenyekiti wa baraza la waislamu nchini Uingereza alisema kuwa si kweli kwamba hakuna mtu ambaye angejitolea kuupokea na kuuzika mwili wa Osama bin Laden. Imamu Sajid alisema kuwa lazima kungekuwepo na mtu ambaye angejitolea kumzika kati ya ndugu zake wengi au mmoja wa watu wanaoshabikia itikadi zake za kigaidi. Naye profesa wa sheria za kiislamu katika chuo kikuu cha University of Jordan, Mohammed Qudah alisema kuwa kumzika mtu baharini haikatazwi katika dini ya kiislamu lakini kwa sharti la kukosekana kwa mtu atakayekubali kuipokea maiti na kuizika kiislamu. "Si kweli na wala si sahihi kusema kwamba hakuna mtu katika ulimwengu wa waislamu ambaye angekuwa tayari kuupokea mwili wa Osama bin Laden", alisema profesa Qudah. "Kama familia imekataa kuipokea maiti, ni jambo rahisi katika uislamu, chimba kaburi kwenye ardhi yoyote ile hata porini, isalie maiti na kuizika", alisema mufti mkuu wa Dubai, Mohammed al-Qubaisi alipohojiwa kuhusiana na suala hilo. Marekani katika kutoa maelezo ya mjadala huu imetoa sababu mbili za kuamua kuizika maiti ya Osama baharini, kwanza ili kuepuka kaburi lake kufanywa kama kaburi la shujaa na hivyo kujijengea umaarufu kwa watu wengi kulitembelea. Pili serikali ya Marekani imesema kuwa haikuwa na muda wa kujaribu kutafuta muafaka na nchi zingine kuukubali kuuzika mwili wa Osama bin Laden. | ||
No comments:
Post a Comment