ULANGA ni moja ya wilaya tano za Mkoa wa Morogoro. Wilaya hiyo ina misitu minane ya hifadhi, yenye ukubwa wa hekta 8,582. Misitu hiyo ni chanzo kikuu cha maji kwa wakazi wa wilaya hiyo.
Katika misitu hiyo, msitu wa Mzelezi ndiyo wenye uhifadhi madhubuti, unaofanywa na
serikali kuu, halmashauri ya wilaya na serikali za vijiji vya Isongo na Mzelezi. Msitu huo ni moja ya misitu ya Milima ya Tao la Mashariki, ambayo inatambulika kimataifa kama Urithi wa Dunia.
Msitu huo ni nguzo muhimu katika kukuza na kuendeleza sekta ya utalii wa ndani na nje, kutokana na kuwa na vivutio adimu, ambavyo havipatikani katika eneo lingine duniani. Kwa mujibu wa Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, msitu huo ulianzishwa Julai
30 mwaka 1954 kwa tamko la serikali namba 216.
Ulianzishwa kutokana na kuwepo kwa bioanuwai nyingi. Kutokana na uhifadhi madhubuti,
hivi leo msitu huo una aina 27 za wanyama wadogo, ambapo aina nne ya wanyama hao, zinapatikana katika msimu huo pekee.
Pia, katika msitu huo kuna aina 109 za ndege na pia kuna aina 336 za mimea. Mbali na wanyama na mimea, kuna aina 68 ya miti katika msitu huo, ikiwemo milengalenga na mikoko.
“Miti hii ni moja ya aina nane za mimea, ambayo inahitaji uhifadhi wa karibu. Aina hizi za miti zipo katika kitabu chekundu cha Shirika la Kimataifa la Kuhifadhi Wanyama na Mimea (IUCN) na aina hizi sasa zinakaribia kutoweka”, inaeleza taarifa hiyo ya Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri.
Taarifa inaeleza pia kuwa msitu huo una aina nane adimu za vipepeo, ambao wanahitaji uhifadhi wa karibu, kwa vile wanapatikana pekee katika msitu huo. Wapo pia vyura 'amphibian’ wa aina tatu, ambao hawapatikani katika msitu mwingine wowote.
Vyura hao ni ‘loveridge’s toad, scarlet snouted frog na southern torrent frog”. Pia kuna vyura ‘reptilian’ aina nane, ambapo aina mbili zinapatikana tu katika msitu huo. Hali kadhalika, kuna mapango makubwa yanayofaa kwa utalii na ikolojia, hususani katika eneo la Mbangayao.
Mapango haya ni kivutio kikubwa cha utalii wa ndani na nje. Hata hivyo, licha ya kuwa na
rasilimali nyingi, msitu huo unakabiliwa na changamoto nyingi, kama vile kilimo ndani ya msitu, uchomaji moto ndani na nje ya msitu na uchimbaji wa madini ndani na jirani na msitu.
Changamoto nyingine ni makazi na kuwepo kwa njia za binadamu ndani ya msitu. Uongozi wa wilaya ya Ulanga, umechukua hatua mbalimbali za kulinda na kuhifadhi msitu huo, kwa kushirikisha wananchi.
Hatua hizo ni pamoja na kuendeleza vyanzo vya maji katika vijiji vya Vigoi na Nawenge. Navyo vijiji vya Isago, Epango, Mkanga, Mdindo, Chikuti na Mzelezi, vina mpango wa pamoja
wa kulinda na kuendeleza hifadhi ya serikali kuu.
Akizungumzia hifadhi za Mkoa huo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Issa Machibya, anasema hifadhi hizo zina ukubwa wa kilometa za mraba 64,000. Machibya anasema kuwa mkoa huo pia una zaidi ya vyanzo 143 vya mito, ambavyo vinahifadhiwa na Serikali kwa kushirikiana na
wananchi.
Anasema, eneo la hifadhi katika mkoa huo ni pamoja na misitu 80 ya hifadhi na mbuga tatu za taifa. Mbuga hizo ni Mikumi na Udzungwa na Pori la Akiba la Wanyama la Selous, lenye umaarufu mkubwa duniani.
Machibya anasema mahitaji ya mazao ya misitu, yanaendelea kuongezeka kila siku; na kwamba uongozi wa serikali katika mkoa huo, unaendelea kushirikiana na wananchi katika kulinda na kusimamia maliasili, ikiwemo misitu.
Anasema ulinzi na usimamizi wa maliasili, ikiwemo upandaji miti, ni suala la kudumu na endelevu.
No comments:
Post a Comment